Mnyika Mbunge halali Ubungo

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), jana kilikuwa katika furaha baada ya Mbunge wake wa Ubungo, John Mnyika kuthibitishwa na Mahakama Kuu kuwa Mbunge halali wa Ubungo jijini Dar es Salaam.


Ubunge wa Mnyika ulikuwa unapingwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na aliyekuwa mgombea wa CCM, Hawa Ng’humbi.

Mahakama hiyo jana kupitia kwa Jaji Upendo Msuya, ilitamka kuwa uchaguzi katika jimbo hilo ulikuwa wa halali na kura alizopata Mnyika ni halali.

Aidha, Jaji Msuya alisema maombi ya Ng’humbi kuwa mahakama hiyo ibatilishe matokeo yaliyompa ushindi Mnyika yametupwa kwa kuwa hakuthibitisha madai yake na kutakiwa kulipa gharama za kesi hiyo aliyoifungua mwaka 2010, siku chache baada ya kubwagwa na kijana huyo.

Awali kabla ya kusomwa kwa hukumu hiyo, Mahakama hiyo jana ilijaa wanachama na wapenzi wa Chadema na CCM na kusababisha askari Polisi kufanya kazi ya ziada ya kutanda kila mahali katika mahakama hiyo na katika Barabara ya Kivukoni kuanzia Mahakama ya Rufaa wakiwa na magari ili kuimarisha ulinzi.

Hukumu hiyo ilisomwa na Jaji Msuya mahakamani hapo kwa takribani saa moja na nusu kuanzia saa 4 asubuhi ambapo pia amuru gharama za kesi hiyo kubebwa na Ng’humbi ambaye kabla ya kuwania ubunge mwaka 2010, alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.

Jaji Msuya alisema Ng’humbi katika madai yake yote matano hakuna hata moja alilolithibitisha kama ambavyo sheria inamtaka mdai katika kesi ya uchaguzi, kuthibitisha dai lake bila kuacha shaka yoyote na kutoa ushahidi kuonesha ni namna gani iliathiri matokeo ya uchaguzi.

Alisema Ng’humbi na mashahidi wake aliowaita mahakamani, hawakuonesha wala kuthibitisha madai yaliyowasilishwa hapo kwamba yalitendeka na namna gani madai hayo yaliathiri matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 31, mwaka juzi.

“Nilipata nafasi ya kupitia ushahidi wa kila shahidi pamoja na vielelezo vilivyotolewa mahakamani katika kesi hii, lakini nimeshangaa ni kwa nini mdai hakuleta mahakamani mashahidi ambao walikuwepo katika chumba cha majumuisho ya kura ambako ndiko madai hayo yalikotokea,” alisema Jaji Msuya.

Alisema hakuelewa ni kwa nini watu zaidi hawakuletwa kuunganisha ushahidi wao kuthibitisha madai ya mdai na kuhoji kama kweli madai hayo yalitokea, ni kwa nini wagombea wengine au watu waliokuwa katika chumba cha majumuisho hawakulalamika?

Katika madai ya Ng’humbi ya dosari ya kura zaidi ya 14,000 alizodai hazieleweki zimetoka wapi, Jaji alisema alipata nafasi ya kuhesabu kura walizopata wagombea wote wa vyama vilivyogombea jimbo hilo ambavyo ni 16 na kubaini ilikuwa ni kosa tu la kibinadamu na halina uhusiano wowote na mdaiwa wa pili, Mnyika.

Kwa mujibu wa Jaji Msuya, fomu namba 24 b ilikuwa na dosari na ndiyo ilikuwa inabishaniwa na Ng’humbi kwa kuwa ilikosewa kuandika.

Alisema Mnyika alitangazwa kuwa ni mshindi baada ya kupata kura 66,742 wakati Ng’humbi alipata kura 50,544 na wagombea wote kuwa kura 132,496.

Jaji Msuya alisema katika ushahidi wa Ng’humbi, hakuonesha ni vipi ongezeko hilo la kura liliathiri matokeo ya uchaguzi na vipi Mnyika alihusika na ongezeko hilo.

Kabla ya kuanza kuchambua hoja za Ng’humbi, Jaji Msuya aliwapongeza mawakili katika kesi hiyo ambao walijitahidi kuwasilisha mashahidi na kuhoji maswali ya msingi.

Alisema mawakili hao hawakupoteza muda kwa kuuliza maswali yasiyo na msingi wala kuwasilisha pingamizi zinazosababisha shauri kuwa na mlolongo mrefu.

Mnyika aliwakilisha na wakili Edson Mbogoro wakati wakili wa Ng’humbi alikuwa Issa Maige na Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliwakilishwa na Justus Mlokozi.

Kuhusu madai ya Ng’humbi kuwa alidhalilishwa kwa kuitwa fisadi na Mnyika katika mkutano alioufanya katika kampeni kwamba aliuza nyumba ya Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania (UWT), na kwamba watu wasichague CCM inakumbatia mafisadi, Jaji Msuya alisema hayakuwa na ushahidi.

Alifafanua kwamba Ng’humbi alidai maneno hayo yalizungumzwa na Mnyika katika mkutano uliokuwa na watu zaidi ya 500, lakini yeye hakuwapo. Kutokana na kukosekana kwa uwepo wake, Jaji Msuya alisema Mahakama haichukui maneno ya kuambiwa, bali mtu aliyesikia mwenyewe au kushuhudia.

“Katika watu wote hao 500 waliokuwa katika mkutano huo, hakuja hata mtu mmoja kutoa ushahidi na pia haikuthibitishwa ni namna gani iliathiri uchaguzi na hivyo hoja hiyo imeondolewa,” alisema Jaji Msuya.

Kuhusu madai kwamba Mnyika aliingia na wafuasi wengine wa Chadema katika kujumlisha matokeo, Jaji Msuya alisema ushahidi pekee ni wa Ng’humbi na kwamba hadhani kuwa ni jambo linalowezekana mtu asiyehusika kuingia katika chumba cha majumuisho ya kura wakati kulikuwa na ulinzi.

Alisema mbali na ulinzi, hata wagombea wengine wangelalamikia jambo hilo, lakini Ng’humbi hakuleta mashahidi waliokuwa katika chumba hicho kutoa ushahidi kuwa kuna watu wasiohusika waliingia.

Kuhusu madai kuwa Msimamizi wa Uchaguzi alitumia kompyuta za mkononi (laptop) za Mnyika badala ya kompyuta rasmi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na pia hazikukaguliwa kiasi cha kutia shaka kuwa pengine kulikuwa na taarifa zisizo rasmi katika kompyuta hizo ikiwa ni pamoja na ongezeko lile la kura 14,000, Jaji Msuya alisema ushahidi umeonesha kuwa kompyuta hizo hazikutumika.

Alifafanua kwamba kompyuta zilizotumika zilikuwa za mawakala na kwamba katika madai hayo, Ng’humbi angeweza kuleta mashahidi zaidi kuthibitisha akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi, Rajab Kiravu.

“Tofauti ya kura kama nilivyosema nimepiga hesabu na nimeona kuwa ni matatizo ya kibinadam na hakuna athari yoyote katika matokeo ya uchaguzi, ni shahidi wa tatu pekee aliyekuja kutolea ushahidi hili na Ng’humbi angeweza kuleta mashahidi zaidi,” alisema Jaji Msuya ambaye alianza kuisikiliza kesi hiyo kuanzia Aprili 19, mwaka huu na majumuisho ya pande zote yalifanywa Mei 4, mwaka huu.

Baada ya hukumu hiyo, Mnyika alikumbatiana na Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye alikuwapo mahakamani hapo. Pamoja walitoka nje, Mnyika akiwa amebebwa na wafuasi wa Chadema wakiimba na kushangilia kwa ushindi huo.

Hata hivyo, hakukuwa na vurugu kubwa zilizokuwa na madhara zaidi ya maandamano yaliyoondoka mahakamani hapo wakiimba.

Mbowe aliwaeleza waandishi wa habari kuwa kesi hiyo imetumia zaidi ya Sh bilioni mmoja na kutaka kabla ya kusikiliza kesi kama hiyo, uchunguzi ufanyike kwanza ili ikionekana haina hoja za msingi, itupwe mapema.

“Mahakama imetenda haki na hii inaonesha namna ambavyo inaweza kutenda haki hata katika vyama vya upinzani,” alisema Mbowe.

Naye Ng’humbi alisema amepokea uamuzi uliotolewa, lakini hawezi kusema lolote kwa sasa na kuwataka wana CCM wawe na utulivu kwa sababu anaamini ni watulivu na kama kuna jambo tofauti, atazungumza baadaye.

Hadi sasa, Mahakama imekwisha kutengua matokeo ya ubunge ya mwaka 2010 katika majimbo mawili pekee, Arusha Mjini kwa Godbless Lema wa Chadema na Sumbawanga Mjini lililokuwa la Aeshi Hilary wa CCM.

Majimbo ambayo kesi zao zilitupwa na mahakama na wabunge wake kuendelea na nafasi zao ni Segerea, Kasulu Mjini, Biharamulo, Singida Mashariki, Ilemela, Nyamagana, Kilwa Kusini, Muhambwe na Meatu.

0 comments

Leave a Reply