KATIBU wa Itikadi na uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Nape Nnauye ametajwa kuwa gamba namba moja linalotakiwa kuvuliwa, kwa kile kilichodaiwa kutoa matamshi mengi ambayo yamekivunjia heshima na kukidhohofisha chama hicho.
Nape pia ameshutumiwa kwa kushindwa kwake kubuni mbinu za kuingiza wanachama na zaidi kupambana na wimbi la kuhama kwa viongozi, makada na wanachama wa CCM.
Shutuma hizo nzito zimetolewa na Mbunge wa Jimbo la Msalala wilayani Kahama mkoani Shinyanga, Ezekiel Maige (CCM) jana wakati akizindua matawi mawili ya wakereketwa wa chama hicho ambao ni wajasiriamali, katika Kijiji cha Isaka wilayani hapa.
Maige alisema kuwa Nape amekuwa akitoa kauli ambazo si za msingi, zisizojenga bila kujua kuwa zinakidhohofisha chama hicho tawala.
Mbunge huyo ambaye amepata kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, alisema kwa sasa kuna wimbi kubwa la wana CCM wanaohamia vyama vya upinzani, ambalo ilitegemewa kuwepo kwa juhudi za makusudi za kuzuia chini ya usimamizi wa katibu huyo wa itikadi na uendezi.
“Kitendo cha CCM kupoteza wanachama zaidi ya 1,000 kwa wakati mmoja mkoani Arusha na sehemu nyingine wanachama 3,000, kinashitua, na ilitegemewa Nape kusimama imara na kuhakikisha chama hakiendelei kupoteza wanachama wake, lakini ndio kwanza anasema hajali na eti hao ni makapi,” alisema kwa kushangaa.
Nape akihutubia vijana mjini Bukoba siku chache zilizopita, alidai kuwa hata kama wanachama wote watahama, yeye (Nape) atabaki peke yake na CCM haitakufa.
Alidai kuwa kasi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) haiwezi kupuuzwa na kiongozi makini, na kuongeza kuwa zinahitajika busara na bidii za kuwapa moyo waliopo ili nao wasiondoke na si kuwasimanga.
“Jamani Nape anachokifanya sasa ndani ya chama mimi ninaweza kuamini kwamba anatumika na kukidhi matakwa ya waliomtuma na si manufaa ya chama.
“Ninalolisema hapa lisitafsiriwe kwamba nalilia uwaziri, hapana, ila ni uchungu nilionao kwa chama changu kuona kila siku tunavyopoteza idadi kubwa ya wanachama, tuliyemkabidhi jukumu la uenezi anasema hajali, sasa huyu si atupishe mapema kabla mambo hayajaharibika?”
Maige alimwomba Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja kutumia nafasi yake kuwashauri wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kuchukua hatua za haraka dhidi ya Nape.
Wakati Maige akitoa maneno hayo mazito, Mgeja alikuwa ameinamisha kichwa chake chini, lakini mamia ya wana CCM pamoja na wananchi wengine walishangilia kwa nguvu.
Katika hatua nyingine, Maige aliwalaumu viongozi wa CCM katika ngazi ya wilaya na kata, ambao wamekuwa na tabia ya kutowatembelea wananchi na kusikiliza kero zao, wakisubiri mpaka viongozi wa kitaifa.
Alisema tabia hiyo ni moja ya vyanzo vya wananchi kuichukia CCM.
“Jamani inakuwaje kiongozi mwenezi wa CCM kata ama wilaya anakaa kimya kabisa, hakuna kazi yoyote ya uenezi anayoifanya, hata kama katika kata ama wilaya yake itakuwa imetembelewa na wapinzani na wakamwaga sumu, wao hawajibu, wanasubiri mbunge ama diwani aitishe mkutano na wao hujitokeza,” alisema.
Alisema ili kukabiliana na wimbi la mabadiliko, ni vizuri wana CCM wakakaa chini na kujipanga vizuri kwa kuwa kitu kimoja badala ya kugawanyika kutokana na maslahi binafsi.
0 comments