Engaruka:Kabila lililotoweka kimiujiza

WATAFITI wa mambo ya kale wanapofika eneo la Engaruka, mkoani wa Arusha hujiuliza, “kabila lililokuwa likiishi hapa lilikwenda wapi?”

Hata hivyo hadi leo hakuna mtu mwenye jibu sahihi hivyo kabila hilo liko kwenye orodha ya makabila yaliyopotea. Watu wa Engaruka walikuwa wakiishi kwenye bonde la ufa eneo
lililopo kati ya Ziwa Manyara na Ziwa Natroni karibu na Kreta ya Ngorongoro.

Inaaminika kuwa kabila hilo, liliishi eneo la Engaruka kuanzia karne ya sita lakini utafiti za
hivi karibuni zinaonesha kuwa waliishi eneo hilo kuanzia zama za chuma mwanzoni mwa karne ya 15.

Utafiti uliofanywa na wataalamu wa mambo ya kale na watafiti wa mambo ya akiolojia hususani John Sutton, unaonesha kuwa eneo la Engaruka lilikuwa na maelfu ya watu ambao waliishi katika mfumo wa vijiji na walikuwa wakiishi katika vijiji vikubwa saba na mashamba yao yalikuwa na ukubwa wa ekari 5,000.

Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa kabila hilo lilikuwa linajishughulisha na kilimo cha kisasa
cha umwagiliaji pamoja na ufugaji na inakisiwa kwamba lilitelekeza mashamba yao kati ya mwaka 1700 na 1750 na kuhama eneo hilo kutokana na sababu ambazo hadi leo hazijajulikana.

Urithi ulioachwa na kabila hilo ndio unaowafanya wanasayansi kuendelea kulitafuta kabila hilo bila kuchoka. Eneo lililotelekezwa lina miundo imara ambayo inadhihirisha kuwa watu wa kabila hilo walikuwa wakulima stadi wenye vipaji na utaalamu wa hali ya juu katika kilimo
cha mwagiliaji. Pia walifuga ng’ombe, mbuzi na kondoo.

Ingawa kabila hilo lilitoweka miaka mingi kabla ya kuingia zana bora za kilimo, lilikuwa linatumia mbinu bora za kilimo cha kisasa kwa kuwa katika makazi yao kulikuwa na mashamba yaliyotengenezwa kitaalamu kwa lengo la kuzuia mmomonyoko wa udongo.

Inasemekana watu wa Engaruka waliishi katika eneo tambarare lisilofaa kwa matumizi ya kilimo kwa kuwa lilikuwa na ukame na udongo mwepesi mithili ya vumbi jembamba. Hata hivyo, walitumia utaalamu wa hali ya juu na wa kipekee kutengeneza vitalu ambavyo kingo zake zilijengwa kwa mawe.

Pia walichimba mifereji kutoa maji sehemu zenye miinuko na kuyapeleka katika mashamba waliyoyatengeneza kwa ustadi mkubwa. Mirereji hiyo ilijengwa kwa kutumia mawe ili kuzuia maji yasipotee, na iligawanywa na kufanywa kuwa miembamba ili kusambaza maji kwenye mashamba.

Pia waliweka mawe kwenye kingo za matuta ili kuzuia mmomonyoko wa udongo. Waliokuwa wafugaji wa ng’ombe, mbuzi na kondoo walikuwa na utaratibu wa kuweka mifugo yao katika mazizi kisha kuitafutia chakula ili kuepuka mmomonyoko wa udongo unaosababishwa kulisha mifugo mingi katika eneo dogo.

Watu hao walikuwa wakitumia samadi kurutubisha mashamba hivyo walikuwa watunzaji wazuri wa mazingira. Kwa kuwa kabila hilo lilitoweka kabla ya kuanza kutumika kwa mfumo
wa kuweka kumbukumbu kwa maandishi, hakuna mtu anayefahamu watu hao walikuwa wa namna gani na walizungumza lugha gani.

Pia hakuna mwenye uhakika kama kabila hilo lilikuwa likijiita Engaruka. Watu waliofika eneo hilo waliamua kusema ni kabila la Engaruka kwa sababu eneo hilo lilikuwa likiitwa Engaruka.

Mwandishi wa Kitabu cha Makabila ya Kaskazini Mashariki mwa Tanzania, Gervase Mlola, anasema kuwa baadhi ya watu wanasema jina la Engaruka linatokana na asili ya neno la Kimaasai “ng’aruka” likiwa na maana ya sehemu kame au jangwa.

Inasemekana kuwa baada ya Wamasai kuhamia eneo la kusini, waliamua kuita eneo hilo Engaruka, kwa sababu walilifananisha na jangwa. Pia wapo wanaoamini kuwa jina la Engaruka linatokana na neno la kisukuma “Wangaruka”, ikiwa na maana salamu za asubuhi.

Inasemekana kuwa eneo hilo, lilikuwa kituo cha mapumziko cha Wasukuma, ambao walikuwa wakisafiri kutoka kanda ya Ziwa kwa ajili ya kukutana na wafanyabiashara waliokuwa wakitokea Mashariki.

Hata simulizi za Wasukuma hazioneshi kuwa waliwahi kukutana na watu wa Engaruka wakati wakiwa katika safari za kibiashara.

Mhifadhi Mkuu wa mambo ya akilojia katika Makumbusho ya Taifa na Nyumba ya Utamaduni, Amandus Kwekason anasema inaaminika kuwa kabila hilo lilitoweka na haijulikani liliko kwa sababu sio rahisi kabila linalokaa katika mfumo wa vijiji kubadilisha kabisa mfumo wa maisha na kuanza utamaduni mpya.

“Ingawa hivi sasa Wamaasai wanaishi eneo la Engaruka ni wazi kuwa Wamasai sio watu wa asili wa Engaruka kwa sababu sio wakulima. Wapo wanaodai kuwa kabila la Wairaqi linatokana na watu wa kale wa Engaruka lakini utafiti wa kisayansi unaonesha kuwa zana na
utamaduni wa kabila la Wairaq unatofautiana na ule wa Engaruka,” anasema Kwekason.

Anasema watu wanaoweza kubadilisha mfumo wa maisha ni watu waliotekwa na kupelekwa
utumwani kisha kuchanganywa na jamii nyingine na kulazimishwa kufuata mfumo na utamaduni wa watu wengine.

Hivyo inaaminika kuwa kabila la Engaruka lilitoweka kwa sababu zinazotokana na wao
wenyewe kwa kuwa Tanzania haina historia ya kabila nzima kutekwa au kupelekwa utumwani.
Kwekason anasema utafiti wa kina uliweza kukusanya vipande 5,280 vya masalia ya watu wa Engaruka ikiwa ni pamoja na mifupa na zana mbalimbali zilizotumika kwenye karne ya 15.

Masalia yamehifanyiwa katika Makumbusho ya Taifa na Nyumba ya utamaduni jijini Dar es
Salaam na hutumika kuendelea kufanya utafiti wa kutafuta kabila hilo kwa kuoanisha zana za watu hao na zana na makabila mbalimbali Tanzania na nchi jirani.

Pia utafiti umefanyika kwa kuangalia kwa kina miundo ya watu wanaojihusisha na kilimo cha umwagiliaji lakini hakuna mfumo inayofanana na ile iliyoachwa Engaruka. Ingawa wataalamu hawajajua sababu ya watu hao kuhama, kuna sababu mbalimbali zinazokisiwa.

Mosi inakisiwa kuwa huenda walikimbizwa na Wamaasai kwa sababu watu hao walitoweka karne ya 17 kipindi ambacho Wamasai walihamia maeneo ya Kusini na kufika eneo hilo la Engaruka.

Inakisiwa kuwa huenda watu wa Engaruka walihofia kwamba wageni waliofika na mifugo mingi wangeharibu mashamba yao jambo lililosababisha kuhama. Hata hivyo hakuna ushahidi
kwamba Wamaasai walivamia watu wa Engaruka kwa sababu katika simulizi za historia ya kale hakuna sehemu ambayo Wamasai wanataja watu wa Engaruka.

“Kwa kuwa historia ya kale ilikuwa ikihifadhiwa kwa njia ya simulizi, inaaminika kuwa Wamaasai hawakuwahi kukutana na watu wa Engaruka ndio maana simulizi zao hazitaji watu wahao,” anasema Kwekasoni ambaye pia ni mtalamu wa mambo ya akiolojia.

Pia ushahidi unaonesha kuwa wamasai wana uwezo wa kuishi na wakulima hivyo isingekuwa rahisi kwa watu hao kutoweka kabisa kwa sababu ya kugombana au kuhofia kuishi na wamaasai.

Wapo wanadhani kwamba watu wa Engaruka walitelekeza mashamba yao kutokana na
mabadiliko ya tabia nchi yaliyolikumba eneo la Kusini mwa Ikweta. Inasemekana kuwa
katika karne ya 15 na 16 mito inatiririka maji wakati wote ilikauka kutokana na ukame
uliojitokeza karne ya 17 na 18, kipindi ambacho watu hao walitoweka.

Hata hivyo, sababu ya ukosefu wa maji haijaweza kuthibitishwa kwa sababu bado kuna makabila mengine yanayokaa katika maeneo ya jirani kama Wasonjo na Wairaqi.

Wataalamu wa masuala ya mazingira wanasema mabadiliko makubwa ya mazingira yanaathiri jamii za watu wengi hivyo isingewezekana mabadiliko hayo kuathiri watu wa Engaruka pekee na kuacha makabila mengine yanayoishi karibu na eneo hilo.

Pia wapo wanaodai kuwa huenda watu wa Engaruka walikabiliwa na tatizo la ongezeko la watu hivyo waliamua kuhama kwa lengo la kutafuta ardhi kubwa ili kuendeleza kilimo cha umwagiliaji.

Hata hivyo, sababu hivyo imepingwa kitaalamu kwa sababu hadi leo hakuna anayefahamu walikokwenda.

Utafiti uliofanywa na Louis Leakey mwaka 1935, Hamo Sasson mwaka 1964, na mwaka 1966, Peter Robertshaw na Taasisi ya Uingereza mwaka 1982 unaonesha kuwa baadhi ya utamaduni wa watu wa Engaruka unafanana na wa Wanjo, kabila ambalo linaishi kilometa 100 Kaskazini mwa Ziwa Natron.

Kwa kuwa Wasonjo hawaishi mbali na Engaruka, baadhi ya watafiti walihisi kuwa Wasonjo wanatokana na watu wa kale wa Engaruka kwa kuwa wanajihusisha na kilimo cha umwagiliaji na muundo wao wa kutengeneza mifereji unashabihiana kidogo na ule wa Engaruka.

Hata hivyo, utafiti wa kina unabainisha kuwa Wasonjo hawana utaalamu wa kutumia mawe kuzuia mmomonyoko wa udongo. Pia hawatumii samadi kwa ajili ya kurutubisha mashamba yao.

“Kwa ujumla kilimo cha Wasonjo hakitumii mbinu za kisasa ikilinganishwa na kilimo
kilichokuwepo katika vijiji vya zamani vya Engaruka hivyo ni dhahiri kwamba Wasonjo sio
watu wa Engaruka,” inaeleza ripoti ya utafiti uliofanywa Sutton.

Jambo lingine linalodhihirisha kuwa Wasonyo hawatokani na kizazi cha kale cha Engaruka ni tofauti katika utengenezaji na matumizi ya vyombo hasa vyungu na mitungi pamoja na vyombo vingine vya ndani vilivyotengenezwa kwa kutumia udongo.

Baadhi ya watu walihisi kuwa huenda watu hao walihamia Kilimanjaro Magharibi. Wanasayansi wa masuala ya akiolojia walipiga kambi mkoa wa Kilimanjaro na kufanya utafiti wa kina. Utafiti huo ulibaini kwamba watu wa Kilimanjaro wana baadhi ya mambo yanayofanana na watu wa Engaruka.

Mosi, uhaba wa ardhi umesababisha Wachaga kutunza ardhi yao kama watu wa Engaruka na wanajihusisha na kilimo na ufugaji. Ufugaji wa Wachaga ni kama wa Engaruka, kwa sababu wanakabiliwa na uhaba wa ardhi.

Pia ufugaji wao ni kama wa watu wa Engaruka kwa sababu wanafuga mifugo michache ambayo hufungia kwenye mazizi kisha kuitafutia chakula. Pia wanatumia samadi inayotokana na mifugo hiyo kwa lengo la kurutubisha ardhi yao ya kilimo kama watu wa Engaruka.

Hata hivyo, wanasayansi walibaini kuwa ipo tofauti kubwa katika uandaaji wa mashamba kwa sababu pamoja na kuwa na maji yanayotiririka kutoka sehemu za miinuko, Wachaga hawana utaalamu wa kutengeneza mifereji ya kilimo cha umwagiliaji kama watu wa Engaruka.

Pia, vyombo na mapambo yao ni tofauti na yale ya watu wa Engaruka. Ingawa Wachaga wanakabiliwa na uhaba wa ardhi wamefanikiwa kwenda kutafuta maisha sehemu nyingine ila wana kawaida ya kurudi nyumbani kila mwaka kwa lengo la kudumisha mila na desturi zao, hivyo Wachaga hawana uhusiano na watu wa kale wa Engaruka.

Pia, utafiti kama huo ulifanywa katika jamii ya watu wa kabila la Wapare mkoani Kilimanjaro na katika milima ya Taita nchi ya jirani ya Kenya na matokeo yanaonesha kuwa kabila hilo ni tofauti na Engaruka.

Ufafiti huo ulibaini kuwa katika nchi ya Kenya kuna kabila la Marakweti ambalo mfumo wao wa kutengeneza mirefeji kwa kilimo cha umwagiliaji unashabihiana na ule wa Engaruka.
Kabila hilo linaishi kilometa 400 Kaskazini mwa Kenya katika bonde la Kerio.

Hata hivyo utafiti uliofanywa na Scotsman Thomson unaonesha kuwa kuna tofauti kati ya makabila hayo, hasa kwa kuangalia zana na mapambo yao. Watu wa Engaruka walikuwa
wakitumia shanga kutengenezwa mapambo, pia walivaa mikufu iliyotengenezwa vyuma vizito.

Pia walikuwa na mapambo machache yanayotokana na makasha ya wadudu wa baharini kama vile simbi. Vyungu na mitungi yao ilitengenezwa kwa ustadi mkubwa na katika mtindo tofauti na makabila mengine yaliyoishi jirani na Engaruka.

Ingawa kabila la Engaruka lilitoweka, liliacha urithi ambao unatumika na wanasayansi hadi
leo. Mfumo wao wa kilimo cha umwagiliaji ni kielelezo kuwa Waafrika wana utaalamu wa kijadi katika kilimo cha umwagiliaji na kwamba utaalamu huo haukuletwa na ukoloni.

Kutoweka kwa kabila hilo ni changamoto hasa kwa wanasayansi na watafiti wa mambo ya kale. Taarifa za tafiti mbalimbali zilizofanyika kwa zaidi ya miaka 100, hazijaweza kubaini watu wa kabila hilo wako wapi na kwa nini walitelekeza makazi yao ya asili.

Kutoweka kwa kabila hilo ni changamoto kwa makabila mengine ambayo yanaacha utamaduni wao wa asili.

Kwa kuwa binadamu ana shauku ya kujua asili yake ni vyema akabila kujitahidi kutunza kumbukumbu hasa kuwafundisha watoto lugha za asili, na kuweka rekodi za makabila hasa kipindi hiki ambacho Tanzania imeingia kwenye mfumo wa utandawazi ambao unasababisha watu wengi kuacha kutumia zana za asili na kutumia zana zilizotengenezwa na mataifa ya Magharibi.
more information visit: http://www.habarileo.co.tz/makala 

0 comments

Leave a Reply