Boma la Mjerumani Mikindani ni kivutio



Jengo hili lilikuwa ofisi ya Mjerumani lakini sasa limegeuzwa kuwa hoteli
Na Charles Kayoka
Nilifika Wilaya ya Mikindani, mkoani Mtwara kwa mara kwanza miaka kumi na nne iliyopita. Nilipofika Mikindani kwa lengo la kuona majengo ya kihistoria niliona mengine bado yanaweza kukarabatiwa.

Katika safari hiyo nililiona boma la Mjerumani, ambalo lilionyesha kuwa ni kivutio kwa watalii wengi, lakini kasoro  iliyojitokeza halikuwa likitunzwa vizuri sana.Lakini ukienda leo hali ya jengo hilo siyo ile niliyoiona awali. Jengo limechukuliwa na wazungu walioligeuza kuwa hoteli. Kwa kweli linatunzwa vizuri sana. Na kilichofanyika ni kujitahidi kulirudishia kama lilivyokuwa awali. Linavutia na kwa kweli sio tena lile jingo chafu la Boma la Mjerumani kama unavyoyaona mengine ambayo hayatunzwi katika maeneo mbalimbali nchini.

Kutokana na hali hiyo nilijiuliza kwamba tunataka kutunza majengo yetu ya historia kwa kusubiri ufadhili kutoka nje tu!

Jambo la ajabu zaidi, Serikali imekuwa ikiwapa wananchi majengo ya kihistoria  amabayo wanayabomoa na kujenga ujenzi wanaoutaka. Historia inafutwa, kumbukumbu zinafutwa, na hakuna anayejali. Tumekaa tu!.
Serikali inazungumzia kuhifadhi na kukuza vivutia vya utalii. Ni utalii upi? Inasema kuwa inataka kuhimiza utalii wa ndani. Ni utalii upi?

Kama hata vivutio vilivyoko karibu na wananchi havitunzwi, tutawasaidia vipi watalii (wananchi) wa ndani ambao wamekuwa wakishindwa kutembelea mbuga zetu na vivuti vingine?
Tunapowaachia wageni uwezekano wa wananchi kufika katika majengo ya kihistoria ambayo yamegeuzwa kuwa hoteli ni mdogo kwa kuwa watahofia kuwapo kwa gharama kubwa  za kuingia hapo.

Nilifika Unguja na kutembelea makazi ya Sultan Seyd Barghash kuna makazi yaliyodumu kwa miaka zaidi ya mia sasa. Kuna miembe mingi yenye umri mkubwa sana tangu yalipopandwa na sultani huyo.

Nilidhani Serikali ingetafuta fedha na kuboresha bustani ya Unguja na kukarabati jengo la Barghash na kuweka huduma za buradani. Watalii na wananchi, na hasa wanafunzi, wangeweza kufika hapo na kujifunza mengi kuhusu historia ya taifa hili. Lakini jengo lile la Barghash linapotea na kuharibika kadri siku zinavyokwenda.

Kutokana na hali hiyo miaka 10 ijayo jingo hilo halitakuwapo. Nilifika Ras Mkambuu Pemba ambako kuna historia ya taifa tangu miaka mingi tangu Kuzaliwa kwa Yesu Kristo, historia inayotuunganisha na Wairan,(Washiraz kutoka Iran kusini), lakini majengo, makaburi, misikiti na visima vinapotea na siyo muda mrefu vitamezwa na maji ya bahari. Hakuna mtu anayejali.

Wahifadhi watakuambia wanahangaika kutafuta wafadhili kutoka nje ili wawasaidie kutunza historia ya Tanzania. Kweli wageni wanakusaidia kutunza historia ya Taifa!
Kutokana na hali hiyo tutaandika katika vitabu vyetu vya historia kuwa majengo hayo yalijengwa na wageni, na yakaokolewa na wageni. Kila jengo limeokolewa na wageni.

Historia ikiandikwa na wageni maana yake ni kwamba hatujui tunakotoka na wapi tunakokwenda.
source: mwnanchi.co.tz

0 comments

Leave a Reply