POLISI KIGOMA WAOKOA WATATU WANAOTUHUMIWA KWA UCHAWI

 BAADHI YA WANANCHI WAKISHANGAA BAADA YA FAINES KUZINDULIWA NA MTOTO MWENYE MIAKA KUMI ALIYEKABIDHIWA MIKOBA NA MAMA YAKE

 FAINES AKIPAKIWA KATIKA GARI YA POLISI
 FAINES ZAWADI-BINTI ALIYEFARIKI KWA MUDA NA KUREJESHWA DUNIANI AKIWA AMESHIKILIWA NA NDUGU ZAKE
MJUKUU BATROMEO BRUNO NA BIBI YAKE EVANIA SEPHANGA WAKISHUKA KATIKA GARI LA POLISI BAADA YA KUFIKISHWA KITUO CHA POLISI CHA KATI CHA KIGOMA


Na Pardon Mbwate na 
Felister Chubwa, wa Polisi Kigoma
Jeshi la Polisi mkoani Kigoma limefanikiwa kuwaokoa watu watatu waliokuwa wamezingirwa na kundi la wananchi wakitaka kuwaua kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya ushirikina.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoani Kigoma SSP Joseph Konyo, aliwataja watu hao waliokolewa kuwa ni Evania Sephanga(50), mkazi wa wilaya ya Kibondo, Bruno January(46), mkazi wa kijiji cha Nyamhoza na mtoto mmoja mwenye umri wa miaka kumi na mkazi wa kijiji cha Nyamhoza Kigoma mjini ambaye jina lake linahifadhiwa.

Kamanda Konyo amesema kuwa wiki iliyopita majira ya saa tisa mchana, watu hao walizingirwa na kundi hilo kwa madai kuwa walimroga na kumuua msichana mmoja aitwaye Faines Zawadi(20) mkazi wa kijiji hicho cha Nyamhoza ambaye siku moja kabla ya kifo chake alionekana kama mtu aliyechanganyikiwa na kuwa kama kichaa.

Alisema katika tukio hilo, bibi kizee mmoja ambaye alikuwa mshirika wa kundi la waliodaiwa kuwa wachawi, alifanikiwa kutoroka katika mazingira ya kutatanisha alipojifanya kuwa anakwenda kujisaidia.

Kamanda Konyo amemtaja bibi huyo aliyefanikiwa kutoroka kuwa ni Bibi Editha Dosiyo mkazi wa kijiji hicho ambaye baadaye alipatikana na kuhojiwa kabla ya kukabidhiwa kwa Idara ya ustawi wa jamii baada ya kuonekana kuwa maisha yake yangekuwa hatarini.

Amesema baada ya Polisi kupata taarifa za tukio hilo, walikimbia na kwenda kuwaokoa kutoka katika mikono ya kundi la wananchi lakini wakiwa wameshaadhibiwa kwa kupigwa  kiasi.

Habari zinasema kuwa, baadhi ya wananchi walipata taarifa kutoka kwa mtoto aliyeokolewa akisema kuwa baadhi ya watoto waliofariki kijijini hapo, akiwataja (majina tunayahifadhi) alikuwa akiwaona nyumbani kwao nyakati za usiku wakiosha vyombo na baadaye kupewa chakula.

Siku ya tukio hilo, baadhi ya wananchi walisema kuwa kabla ya bibi huyo kutoweka alimnong’oneza jambo mjukuu wake ili amfanyie marehemu ikiwa ni pamoja na kumruka mara saba kisha bibi huyo alitoweka akijifanya anakwenda kujisaidia.

Walisema mara baada ya bibi huyo kutoweka, mtoto huyo wa kiume ambaye ni miongoni mwa waliozingirwa wakitaka kuuawa, alianza kutekeleza maagizo ya bibi huyo na alipomaliza kitendo cha kumruka kwa mara ya saba, msichana yuyo ambaye alikuwa 'mfu' alizinduka na kuomba uji.

Wamesema msichana huyo  alipewa uji na kunywa kisha akapelekwa hospitalini ambako hadi sasa hali yake inasemekana kuwa inaendelea vizuri.
 
Hata hivyo Kamanda Konyo ametoa wito kwa wananchi kuacha kuchukua sheria mkononi na badala yake watoe taarifa Polisi kwa kila jambo wanaloliona kuwa linaweza kuleta uvunjifu wa amani ili hatua za haraka zichukuliwe dhidi ya wahusika.

Mwezi uliopita watu wawili mke na mume, waliuawa na kundi la watu wenye hasira kisha miili yao kuchomwa kwa moto mkoani Kigoma baada wa kutuhumiwa kuwa walikuwa ni wachawi.

0 comments

Leave a Reply