Vipaumbele vya bajeti ya Upinzani!

Waziri kivuli wa Fedha na Uchumi, Zitto Kabwe  akitoa taarifa ya vipaumbele vya Kambi ya Upinzani Bungeni katika bajeti ya mwaka wa fedha 2012/2013.


KAMBI ya Upinzani Bungeni imetangaza Bajeti mbadala kwa mwaka wa fedha 2012/13 yenye vipaumbele 10, kikiwamo kinachoitaka Serikali kuhakikisha inapunguza misamaha ya kodi hadi asilimia moja.Pia kambi hiyo imeainisha namna ya kukabiliana na mfumuko wa bei kwa kuhakikisha inawekeza zaidi katika chakula na nishati, ambapo kwa upande wa chakula iruhusu mchele kuingizwa nchini bila kodi ili kupunguza gharama za maisha kwa wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri Kivuli wa Fedha, Kabwe Zitto, alisema kambi hiyo imebaini kuwa kiwango kikubwa cha misamaha ya kodi cha asilimia tatu kinaweza kupunguzwa, kama nchi nyingine duniani zinavyofanya na fedha hizo kuingizwa kwenye Bajeti ya Taifa.Kambi hiyo inataka maelezo ya kina ya sababu ya Serikali hadi sasa kushindwa kutekeleza ahadi yake iliyoitoa bungeni kuwa misamaha ya kodi itapunguzwa hadi asilimia moja ya Pato la Taifa. 

Pamoja na hayo, alisema kambi hiyo imepanga kukabiliana kikamilifu na mfumuko wa bei ambao uko juu, kutokana na kupanda kwa bei za vyakula ambapo, itahakikisha inapunguza kodi kwenye bidhaa za mafuta ya petroli na dizeli. 
Vipaumbele hivyo ni: 
  • Kuhakikisha fedha nyingi zinaelekezwa katika rasilimali fedha kwenye maendeleo vijijini, hasa kujenga miundombinu ya barabara za vijijini, hatua itakayosaidia wakulima kuuza bidhaa zao kwa bei ya chini jambo linaloweza kupunguza umasikini.
  • Kusimamia wigo wa kutoza tozo la ujuzi (SDL) ambapo sasa waajiri wanalipa asilimia sita ikiwamo Serikali na mashirika ya umma. 
  • Kushusha kima cha chini cha Kodi ya Mapato (PAYE) hadi asilimia tisa ili kuwawezesha wafanyakazi wa kima cha chini kumudu maisha hasa mfumuko wa bei. 
  • Kuongeza mapato ya ndani na kupunguza mikopo ya kibiashara. Alisema katika eneo la mapato ya ndani, kambi hiyo inataka yafikie asilimia 20 ya Pato la Taifa pamoja na kuongeza nguvu za kisheria na udhibiti ili Mamlaka ya Mapato (TRA) ikusanye zaidi kwenye kampuni za simu na katika shughuli za uchimbaji wa madini, mafuta na gesi. 
  • Kupunguza na kufuta kodi kwenye bidhaa za vyakula kwa muda maalumu, ili kushusha mfumuko wa bei kwani sasa ni asilimia 26 hivyo ni muhimu Serikali ikaruhusu wafanyabiashara wakaagiza mchele kutoka nje kwa miezi mitatu. 
  • Kuweka mfumo mpya wa elimu kwa kushirikisha sekta binafsi kutoa elimu bora zaidi ikiwamo kuundwa kwa chombo cha udhibiti wa sekta hiyo. Alimpongeza Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa, kwamba amekuwa akionesha uungwana na usikivu na kumtaka apokee maoni ya Kambi ya Upinzani si kwa maslahi ya upinzani, bali kwa manufaa ya Watanzania.

Mwelekeo wa bajeti hiyo ya upinzani unakuja wakati Serikali imeshatoa mwelekeo na vipaumbele vyake mwishoni mwa wiki iliyopita, ambapo inatarajia kutumia Sh trilioni 15; matumizi ya kawaida yakiwa Sh trilioni 10 na maendeleo ni Sh trilioni tano. Kwa mujibu wa Dk Mgimwa, vipaumbele vya bajeti hiyo ni miundombinu ambayo imegawanywa katika makundi ya reli, umeme, maji salama, usafirishaji na uchukuzi ambavyo vimetengewa Sh trilioni 4.5 na vingine ni kilimo, viwanda, rasilimali watu, huduma za jamii, utalii, biashara ya ndani na nje na huduma za fedha

0 comments

Leave a Reply