Wakuu 10 wa sekondari kushtakiwa

NAIBU Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo ameamuru kukamatwa na kushitakiwa kwa wakuu wa shule 10 za sekondari mjini Kigoma Ujiji ambao wamebainika kuruhusu wanafunzi 391 waliofeli mitihani yao ya kumaliza elimu ya msingi, kuendelea na masomo ya sekondari.

Mulugo alisema hayo kwa nyakati tofauti akiwa katika ziara ya siku mbili mkoani hapa na kuongeza kuwa baada ya hatua ya awali ya kuwavua madaraka ya ukuu wa shule na uchunguzi kufanywa na tume mbalimbali, imethibitika kuwa wakuu hao walihusika na vitendo hivyo.

Alisema walifanya vitendo hivyo kinyume na Sheria ya Elimu namba 25 ya mwaka 1978 na marekebisho yake ya mwaka 2002, huku wakijua vitendo hivyo ni kosa kwa mujibu wa sheria za uendeshaji shule za sekondari.

Akizungumza katika sekondari ya Kasingirima, Naibu Waziri alisema kuwavua madaraka ilikuwa ni hatua ya awali ya kinidhamu.

Baada ya hapo, kinachofuata ni kuchukuliwa hatua za kisheria kwa sababu vitendo vilivyofanyika vya kuwadahili wanafunzi wasio na sifa kuendelea na masomo ya sekondari katika mfumo rasmi wa Serikali, ni kinyume cha sheria.

"Hapo kwa haraka haraka kuna makosa mawili tayari yametendeka; moja ni kughushi nyaraka halali za Serikali na kuwaingiza wanafunzi hao, lakini la pili ni vitendo vya rushwa ambavyo vinaonekana kutendeka katika kuwaingiza wanafunzi hao," alidai.

Katika ziara yake jana mjini Kigoma, Mulugo alitembelea shule tano za sekondari zinazotuhumiwa kuhusika na kadhia hiyo ambazo ni Kasingirima, Mwananchi, Katubuka, Masanga na Mlole. Pia alitembelea Chuo cha Ufundi Stadi (Veta) na jioni alikwenda katika mkutano wa majumuisho na viongozi mbalimbali.

Sambamba na ziara katika maeneo hayo pia, Mulugo anatarajia kuwa na mkutano wa hadhara katika viwanja vya Mwanga Centre ambapo pamoja na mambo mengine alipanga kuwaeleza wazazi madhara ya kuwaingiza katika mfumo rasmi wanafunzi waliofeli mitihani ya kumaliza elimu ya msingi.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Kasingirima, Nkanuliye Hamisi, alikanusha kuhusika na kuwaingiza wanafunzi na kujipatia fedha akidai kuwa alishangazwa na kuwapo kwa wanafunzi hao baada ya kufanyika ukaguzi kutoka nje na kuwa jambo hilo lilifanywa kinyemela kwa wanafunzi kuingia bila kusajiliwa.

Hata hivyo, Elisha Zilikana ambaye ni Mkuu wa Shule ya Sekondari Mwananchi, alikiri kuhusika kuingiza sekondari wanafunzi waliofeli mitihani yao ya darasa la saba akidai kuwa jambo hilo lilifanyika kutokana na huruma kwa watu wanaomzunguka huku akiomba kupewa msamaha kutokana na jambo hilo.

Mwishoni mwa mwaka jana, Ofisi ya Mkaguzi wa Sekondari Kanda ya Ziwa Magharibi ilifanya ukaguzi na kugundua uwepo wa wanafunzi 391 wanaoendelea na masomo ya sekondari wakati walifeli masomo yao ya shule za msingi.

Shule hizo za sekondari zilizokumbwa na kadhia hiyo ni pamoja na Mwananchi, Kasingirima, Rusimbi, Kitongoni, Katubuka, Buteko, Wakulima, Mlole na Masanga ambapo wanafunzi waliokuwa wakisoma katika shule hizo, walilazimika kusitisha na masomo.

0 comments

Leave a Reply