RAIS wa Umoja wa Maaskofu Afrika Mashariki na Kiongozi wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Askofu Dk Valentino Mokiwa amesema waumini Wakristo hawaridhishwi na utendaji kazi wa Polisi ukiwemo ufuatiliaji wa matukio ya kuchomwa moto kwa makanisa visiwani Zanzibar.
Akizungumza katika kikao kilichokutanisha viongozi wa Dini na Serikali katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais jana, Dk Mokiwa alisema Polisi imeshindwa kufuatilia matukio ya uhalifu ikiwa ni pamoja na kuchomwa kwa makanisa hayo.
Alisema tangu mwaka jana zaidi ya makanisa 25 yamechomwa moto na hakuna kesi iliyofikishwa mahakamani.
“Matukio mengi ya kuchomwa moto kwa makanisa yamejitokeza Zanzibar tangu mwaka jana lakini hakuna kesi iliyofikishwa mahakamani au mtu aliyekamatwa,” alisema Dk Mokiwa.
Aidha, alisema hadi sasa wafuasi Wakristo wanafanya kazi zao kwa hofu na wasiwasi kwani baadhi ya watu bado wanashambulia nyumba za ibada ikiwa ni pamoja na kurusha mawe.
“Hadi sasa wafuasi wetu wanafanya kazi zao kwa wasiwasi mkubwa hata katika nyumba za ibada kwani wafuasi wenye siasa kali wanarusha mawe katika nyumba za ibada,” alisema.
Dk Mokiwa alisema hakubaliani na kauli za baadhi ya watu kwamba wanaofanya vitendo hivyo ni wahuni, bila hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yao.
Alifafanua, kuwa kama ni suala la Muungano kwa nini watu hao wachome moto makanisa na wasisubiri Tume ya Kuratibu Maoni ya Katiba ili wawasilishe hoja zao kuhusu Muungano.
“Sisi hadi sasa hatuamini kwamba wanaofanya fujo ni wahuni, kama ni wahuni kwa nini wanachoma moto makanisa na kama ni Muungano kwa nini wasisubiri Tume ya Katiba? “Alihoji Askofu Mokiwa.
Mapema Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud akijibu baadhi ya hoja za Baraza la Maaskofu Tanzania, alisema tayari Serikali imeweka ulinzi wa kutosha kwa makanisa yote visiwani hapa.
“Tumeweka ulinzi katika sehemu zote za nyumba za ibada ikiwamo makanisani na Serikali itahakikisha hakuna fujo zitakazojitokeza kwa sasa,” alisema Aboud.
Aliahidi kuwasilisha kwa Rais Dk Ali Mohamed Shein malalamiko yao yote kuhusu vitendo vya kuwadhalilisha Wakristo visiwani huku Tanzania ikiwa nchi isiyo na dini isipokuwa wananchi.
Mapema viongozi hao walitaka kuonana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi (SMZ) kuzungumzia matukio hayo yenye kuashiria uvunjifu wa amani na utulivu.
Hata hivyo Aboud alikiri akisema wapo watu wanatumia vibaya taasisi za kidini kama mwamvuli wa kisiasa katika kuwasilisha hoja zao mbalimbali, yakiwamo masuala ya Muungano na marekebisho ya Katiba
0 comments