Hujuma Sudan, Rage alazwa mapokezi!

Na Ezekiel Kamwaga, Khartoum

*Walishwa lunch saa 10 jioni
*Chakula cha usiku saa sita usiku
*Rage, Kisaka, wanyimwa pa kulala, walala mapokezi
* Wachezaji wajifua kivyao

UONGOZI wa Simba SC unakusudia kuwasilisha malalamiko rasmi kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kutokana na unyama inaofanyiwa nchini Sudan inakosubiri pambano lake dhidi ya Al Ahly Shendi kesho.
Tangu iwasili nchini Sudan juzi, Simba imekuwa ikifanyiwa vitendo visivyo vya kiungwana na wenyeji wake, Shirikisho la Soka Sudan (SAF) na Al Ahly Shendi.

Jana, Simba ilifanyiwa vitendo hivyo kabla ya kwenda katika mji wa Shendi itakakochezwa mechi hiyo na baada ya kufika katika mji huo uliopo takribani kilomita 170 kutoka mji mkuu Khartoum.

Simba iliwasili Shendi majira ya saa mbili usiku kwa saa za Sudan (sawa na saa za huko) baada ya safari ya takribani masaa manne kutoka Khartoum.

Safari ya kutoka Khartoum hadi Shendi ilianza majira ya saa kumi jioni na timu ikafika saa mbili usiku, kwa maana ya masaa manne ya safari ya barabara jambo ambalo ni kinyume cha kanuni za CAF zinazozungumzia umbali usiozidi masaa mawili.
Ingawa kanuni ya CAF kifungu cha 5 (3) kinazungumzia umbali wa kusafiri kwa basi usizidi kilomita 200, Simba inaweza kutuma malalamiko kwamba kutoka Khartoum hadi Shendi ni zaidi ya kilomita 150 kwa vile si haiwezekani kutumia masaa manne kwa umbali huo.

0 comments

Leave a Reply